1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washukiwa wa 'mapinduzi' Ujerumani wafikishwa mahakamani

Mohammed Khelef
29 Aprili 2024

Mahakama mjini Stuttgart imeanza kusikiliza kesi zinazowahusu wanachama wa kundi moja la siasa kali za mrengo wa kulia wanaotuhumiwa kula njama ya kulivamia bunge na kuipinduwa serikali ya shirikisho la Ujerumani.

https://p.dw.com/p/4fJPd
Stuttgart | Kesi ya Reichsbürger
Wanachama wa kundi la Reichsbuerger wakipandishwa mahakamani mjini Stuttgart siku ya Jumatatu (Aprili 29) kwa tuhuma za kula njama ya kupindua serikali ya Ujerumani.Picha: Bernd Weißbrod/dpa-Pool/picture alliance

Wanachama tisa wa kundi hilo linaloongozwa na mfanyabiashara na mwanamfalme, Heinrich XIII Reuss, waliwasili kwenye mahakama ya mji wa kusini magharibi mwa Ujerumani, Stuttgart, wakisindikizwa na maafisa wa usalama siku ya Jumatatu (Aprili 29).

Miongoni mwa washitakiwa hao alikuwamo mwanajeshi mmoja wa kikosi maalum, mbunge mmoja wa zamani wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, mtaalamu mmoja wa anga za juu na mpishi mmoja mashuhuri wa hapa Ujerumani.

Katika kesi hiyo, waendesha mashitaka walikuwa wanawashutumu kwa kupanga kuipinduwa serikali ya Ujerumani. 

Soma zaidi: Polisi ya Ujerumani yawasaka wanachama wa Reichbürger

Maafisa wa usalama walisema wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wamekuwa wakiongezeka kwa kasi na wamekuwa kitisho kikubwa katika taifa hili lenye historia ya siasa za unazi. 

Kutokana na uzito wa kesi yenyewe na haja ya hatua za ziada za usalama, ilibidi kesi hiyo kugawanywa kwenye mahakama tatu tafauti. 

Athari za nadharia za upotoshaji

Reuss, ambaye kama mapinduzi yangelifanikiwa ndiye aliyepangwa kuwa mkuu wa nchi, atafikishwa mahakamani mjini Frankfurt mwezi Mei, ambapo watafikishwa mjini Munich mwezi Juni.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, watuhumiwa hao walikuwa wameathiriwa na mchanganyiko wa nadharia za upotoshaji zinazotokana na vuguvugu la kimataifa la QAnon na kile kiitwacho Reichsbuerger.

Washukiwa 25 wa siasa za mrengo wa kulia wakamatwa Ujerumani

Vuguvugu la Reichsbuerger linawakutanisha pamoja wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wale wanaopigania haki ya kumiliki silaha na ambao wanakataa uhalali wa jamhuri ya sasa ya shirikisho la Ujerumani.

Wafuasi hao kwa ujumla wanaamini kwenye kuendelea kuwapo kwa kile kiitwacho Reich, ama himaya ya Ujerumani ya kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia, chini ya ufalme, na makundi kadhaa yametangaza mataifa yao wenyewe.

"Chuki dhidi ya demokrasia"

Waziri wa Mambo ya Ndani, Nancy Faeser, alisema makundi kama haya ya Reichsbuerger yanaongozwa na kile alichokiita "chuki dhidi ya demokrasia."

Polisi wa Ujerumani wakimshikilia Heinrich XIII Reuss mjini Frankfurt.
Polisi wa Ujerumani wakimshikilia Heinrich XIII Reuss mjini Frankfurt.Picha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

"Tutaendelea kuchukuwa hatua madhubuti hadi tufanikiwe kuiumbua hadharani na kuivunja mifumo yote ya Reichsbuerger." Alisema waziri huyo.

Soma zaidi: Washukiwa 25 wa siasa za mrengo wa kulia wakamatwa Ujerumani

Watuhumiwa waliopandishwa leo kwenye mahakama ya Stuttgart wanashukiwa kuwa ndio tawi la kijeshi la njama hiyo ya mapinduzi, ambalo lilipewa jukumu la kuanzisha vikosi vya ulinzi wa mipaka ya nchi. 

Miongoni mwao alikuwa ni Andreas M., mwanajeshi wa kikosi maalum aliyesemekana kuwa alitumia fursa ya kuwa kwake mwanajeshi kushawishi wengine jeshini.

Kwa mujibu wa wachunguzi, kundi la Reuss linakubaliana na imani kwamba Ujerumani inatawaliwa na wanachama wa kile kiitwacho "dola la siri" na kwamba inaweza kukombolewa kwa msaada wa mtandao wa siri wa kimataifa, unaofahamika kama "muungano wa washirika."

Vyanzo: dpa, AFP